Na Woinde Shizza Michuzi Tv,Arusha
Wakandarasi mbalimbali wanaotengeneza Barabarani kwa kiwango cha Lami katika jiji la Arusha, wametakiwa kuzingatia maelekezo ya mikataba yao inayowataka kutoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mradi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tarafa wa kata ya Themi ,Felisiani Mtahengerwa wakati wa ziara ya Kamati ya siasa ya CCM kata ya Levolosi ya kutembelea na kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.
Miradi waliotembelea ni pamoja na kukagua Barabara zenye urefu mita 585 zinazojengwa katika kata hiyo na kampuni ya ujenzi ya Ravji ya Mjini Moshi,Mkoani Kilimanjaro,Soko la Kilombero pamoja na ukarabati wa kituo cha Polisi cha Kilombero alichobaini kuwa na changamoto kubwa ya kuvuja wakati wa mvua
Felician aliitaka kampuni hiyo ya ujenzi wa barabara kuwapatia ajira vijana waliopo katika eneo la miradi katika kata hiyo bila kujali itikadi zao za kisiasa pamoja na kuikata kampuni hiyo kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa ubora unaohitajika
Akiongea wakati akiwa kwenye soko la Kilombero alisema kuwa serikali inaomba wadau wa maendeleo kuona umuhimu wa kukirabati kituo cha Polisi cha Kilombero kwa kujitolea thamani za ofisi sanjari na ukrabati wa paa na kusaidia ulipaji wa deni la maji kwani kituo hicho kinasaidia katika suala zima la usalama katika eneo hilo.
"Unajua suala hili sio la lazima ni hiyari ya wadau wa maendeleo kuona umuhimu wake kwani kituo hiki kinasaidia sana katika kulinda Mali zao na usalama katika eneo hili hivyo waone umuhimu wa kuisaida serikali kujitolea"
Naye msimamizi wa kampuni hiyo ya ujenzi ya Ravji ,Peter Mahushi alisema atahakikisha kampuni yake inamaliza Kazi katika muda uliopangwa na kwamba ifikapo September 14 mwaka huu watakabidhi Miradi huo.
Alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwa vijana wa kata hiyo kwa kuanza na vijana watano na kuwataka viongozi hao kuwapelekea majina wao wataangalia na kuona wanauwezo kiasi gani na kuahidi kuwa changamoto zote watazifanyiakazi ndani ya muda uliopangwa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM kata ya Levolosi,Tabu Simile amesema kuwa chama cha mapinduzi kimeridhishwa na ujenzi wa miradi ya Barabara kwa kuona thamani ya fedha inayotolewa ikitumika kama ilivyokusudiwa.
Alisema kuwa wao kama chama wameridhishwa kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa ilani na changamoto ndogo walizokutana nazo wanawataka serikali kuhakikisha inazitatua kama ilivyoahidi ndani ya muda kuokoa na kwenda sambamba na kasi ya ujenzi wenye viwango vinavyokubalika.
Miradi hiyo ya ujenzi wa barabara za lami katika jiji la Arusha inatekelezwa kwa kiwango kikubwa na serikali chini ya wakala wa barabara za mijini na Vijijini (Tarura ) jambo ambalo linazidi kuung'arisha mji wa Arusha ,ambapo wananchi wanafurahi kuona kodi wanazotoa zinatumika kuwaletea maendeleo ipasavyo.
Kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi CCM kata ya Levolosi wakitembelea baadhi ya barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami katika kata hiyo inayotekelezwa na serikali.
Post a Comment