Na Annastazia Paul
Jumla ya mashine 23 zinazotumika katika michezo ya kubahatisha zimekamatwa katika maeneo mbalimbali mkoani Shinyanga na kuteketezwa kwa kuchomwa moto kutokana na waendeshaji wa mashine hizo kukiuka kanuni na taratibu za uendeshaji wake.
Akizungumza jana Agosti 23,2019 wakati wa zoezi la kuziteketeza mashine hizo lililofanyika katika dampo la Mwawaza Mjini Shinyanga,Meneja Ukaguzi na Udhibiti kutoka bodi ya Michezo ya kubahatisha Tanzania Sadiki Elimsu alisema kuwa amepata taarifa juu ya uwepo wa mashine hizo kinyume na utaratibu kutoka kwa mkuu wa wilaya na kuanza msako ambao umefanikisha ukamataji wa mashine hizo.
"Hivi karibuni tulipata taarifa kutoka kwa mkuu wa Wilaya ya Shinyanga akitufahamisha kwamba kuna waendeshaji wa michezo ya kubahatisha ambao wanaendesha katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria, baada ya kupata taarifa hizo bodi iliagiza maafisa wake ili kuja kujithibitishia na kuchukua hatua zinazostahili",alisema Elimsu.
Amesema katika maeneo waliyotembelea bodi hiyo iligundua ukiukwaji wa uendeshaji wa mashine hizo hivyo kuzikamata kisha kuziteketeza.
"Tulibaini kwamba kuna baadhi ya waendeshaji wanakiuka mashairi ya leseni ambazo wamepewa ambazo zinataka mashine hizi zifungwe maeneo ambayo tayari bodi imeshafanya ukaguzi wake na kujiridhisha kwamba yanakidhi matakwa ya kisheria, hivyo katika maeneo hayo tuliweza kuzikamata mashine hizo na kuzileta hapa katika dampo hili na kuziteketeza",alisema Elimsu.
Alisema kupitia msako huo bodi imebaini baadhi ya waendeshaji ambao walikuwa wanakiuka taratibu za upatikanaji wa leseni.
"Baadhi ya waendeshaji walikuwa wanachukua leseni kutoka katika Mamlaka ambazo hazina sifa za kutoa leseni za kuendeshea michezo hiyo na tulikuwa tukiwaambia leseni hizo zinatolewa na bodi ya michezo ya kubahatisha Tanzania pekee",alieleza Elimsu.
Ameeleza kuwa baadhi ya mashine zilikuwa zimewekwa katika maeneo ambayo hayakukaguliwa na kuidhinishwa na bodi hivyo kuruhusu hata watoto wacheza jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Katika hatua nyingine Meneja huyo wa ukaguzi na udhibiti kutoka bodi ya michezo ya kubahatisha Tanzania alisema kuna baadhi ya waendeshaji wanaingiza nchini mashine hizo kinyemela na kwambaa mmoja wao ameshakamatwa na yupo jijini Dar-es-salaam akishikiliwa na jeshi la polisi.
"Bado anashikiliwa na jeshi la polisi yeye alipatikana na mashine zinazokadiriwa kuwa ni zaidi ya 1,200 ambazo tayari tumeshazikamata na uchunguzi bado unaendelea kuhusiana na mfanyabiashara huyo",alisema Elimsu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko aliwaomba wananchi kushiriki kwa kutoa taarifa kwenye vyombo husika ili kuweza kuondosha michezo hiyo katika Wilaya ya Shinyanga.
"Wananchi wote tushirikiane, tushikamane, yeyote mwenye taarifa kwa mashine hizi zipo katika, vijiji, katika kata zetu watoe taarifa mapema na tutakuja kuziondosha ili sasa tudhibiti hao watu ambao wanakwepa kulipa kodi yetu ya serikali, kwasababu wanavyoendesha hizi maana yake wanakwepa kodi za serikali na mapato ya serikali yanapotea bure",alisema Mboneko.
"Tutaendelea kuzikamata na tutaendelea kuhakikisha kwamba hawakai tena katika Wilaya yetu ya Shinyanga",alisema.
Amesema kuwa michezo hiyo inasababisha mmomonyoko wa maadili kwa sababu watoto wanaiba kwa wazazi wao, na hata wananchi wengine pia wanapoteza mali zao kwani wanauza mpaka mashamba na chakula kwaajili ya kwenda kucheza michezo hiyo jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akielezea kuhusiana na kukamatwa kwa mashine hizo.
Mashine zinazotumika katika michezo ya kubahatisha zilizokamatwa katika maeneo mbalimbali mkoani Shinyanga Mashine hizo zikiwa katika kituo cha polisi kabla ya kwenda kuteketezwa kwa moto.
Meneja Ukaguzi na Udhibiti kutoka bodi ya Michezo ya kubahatisha Tanzania Sadiki Elimsu akielezea kuhusu mashine zilizoteketezwa kwa moto.
Mashine hizo zikiwa zinawaka moto
إرسال تعليق