Una
mahusiano na mwanaume au mwanamke ambaye kimsingi mpo katika uchumba.
Unampa zawadi nyingi naye anakupa zawadi. Mnayo ahadi ya kufunga ndoa
na kuishi kama mme na mke . Na kwasababu hiyo unajitoa sana kimatumizi
kwa mtu huyo.
Lakini
katika mazingira usiyoyaelewa unaona sasa mambo hayaendi vizuri.
Hayaendi vizuri katika kiwango ambacho sasa mahusiano yamevunjika
kabisa. Hakuna tena mahusiano. Au bado yapo lakini kwa mambo
unayofanyiwa unaona kabisa hutakiwi tena.
Kumbuka
huko nyuma umegharamia sana. Umegharamia kwa fedha na mali. Swali ni je
vitu hivi haviwezi kurudishwa ?. Vitu hivi haviwezi kufidiwa ?. Na je
sheria imeongelea kuhusu jambo hili ?.
Majibu
ya maswali haya yote ni ndiyo. Ni ndiyo, na gharama pamoja nazo zawadi
zinaweza kurejeshwa. Unaweza kushangaa kuona sheria imeongelea hata
mambo ya uchumba lakini ndio ukweli.
Wengi
tunaijua sheria katika kuongelea wizi, dhamana, mikataba, mirathi, ndoa,
na mengine. Lakini ni vyema tukajua kuwa sheria ni pana na imeongelea
mambo mengi mno. Hili la uchumba nalo ni sehemu ya yaliyoongelewa.
1 KUVUNJA UCHUMBA
.
Kifungu
cha 69( 1 ) cha Sheria ya Ndoa iliyofanyiwa marekebisho 2010 kinasema
kuwa mtu anaweza kufungua shauri na kudai fidia baada ya uchumba
kuvunjwa.
Kwa
haraka utaona kuwa tafsiri ya kifungu hiki sio kufungua shauri ili
kumlazimisha mtu akurudie, hapana. Mahakama haiwezi kutoa maamuzi kuwa
fulani lazima amrudie fulani. Isipokuwa lengo lake ni kumtaka yule
aliyeumizwa katika hili kudai fidia kutokana na maumivu aliyoyapata.
Hapa hatujaongelea kurudisha zawadi.
Kudai
fidia na kurudisha zawadi ni vitu viwili tofauti. Fidia inahusu kulipwa
maumivu uliyoyapata kutokana na tukio hilo la kuachwa pamoja na muda
uliopoteza na huyo mtu. Wakati zawadi ni kurejesha kile ulichotoa.
Kwahiyo la zawadi tutaliona baadae.
Aidha
masharti ya kufungua shauri la kudai fidia ni kuwa , moja anayefungua
shauri awe ni yule aliyeumizwa, pili ahadi ya kuoana lazima iwe ilikuwa
imefanyika Tanzania, tatu wakati mnaingia kwenye mahusiano iwe mlikuwa
nyote mmetimiza miaka 18 .
2. KURUDISHA ZAWADI.
Kifungu
cha 71 cha Sheria ya ndoa kinasema kuwa mtu anayo haki ya kufungua
shauri kudai kurejeshewa zawadi ambazo alizitoa kwa mtu ambaye alikuwa
ana ahadi ya kufunga naye ndoa lakini ndoa haikufungwa.
Zawadi
ni pamoja na fedha, nyumba, magari, nguo na kila kitu chenye
thamani(valuable). Haijalishi mali hiyo ipo kwenye jina la nani suala la
msingi ni kuthibitisha kuwa wewe ndiye uliyetoa hiyo zawadi.
Shauri
la namna hiyo unaweza kulifungua mahakama yoyote ya mwanzo, ya wilaya,
ya hakimu mkazi au hata mahakama kuu. Itategemea na thamani ya kiwango
cha mali unazodai.
Kama
mali hizo zitakuwa zimekwishatumika au hazipo tena pengine zimeuzwa au
kutolewa zawadi kwa mtu mwingine basi itatakiwa kulipwa fedha
zinazolingana na mali hizo au mali hizo zikanunuliwe tena kwingine ili
kumrudishia anayedai.
Ukishindwa
kabisa kurudisha basi mali zako binafsi ambazo hazikuwa sehemu ya
zawadi zitauzwa ili kupata kiwango kinachodaiwa na kama huna mali yoyote
ya kuuza utatakiwa kwenda jela kama mfungwa wa madai.
Kwa hiyo watu wanatakiwa waelewe kuwa uchumba na ahadi za kuoana si jambo jepesi kama wanavyolitamka na kuliahidi .
إرسال تعليق