Na WAJMW-DOM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema ugonjwa wa Corona unaelekea kuisha nchini ambapo mikoa zaidi ya 15 haijaripoti mgonjwa yeyote wa Corona kwa zaidi ya wiki.

Waziri Ummy amesema hayo leo wakati alipotembelea kituo cha afya cha Mkonze kilichotengwa kwa ajili ya kuwahudumia watu waliopata maambukizi ya ugonjwa wa Corona jijini Dodoma na kukuta vitanda vikiwa tupu bila kuwa na mgonjwa yeyote kwa zaidi ya wiki.

Waziri Ummy amesema kupitia Waganga wakuu wa Mikoa 15 nchini wamethibitisha kutokua na mgonjwa wa Corona na Mikoa mingine yenye wagonjwa imeripoti kuwa wagonjwa hao wanaendelea vizuri.

Aidha, Waziri Ummy amewashukuru watoa huduma za afya wa kituo cha Mkonze kwa kazi nzuri walioifanya ya kuwahudumia wagonjwa na kuchukua tahadhari zilizosaidia wahudumu hao kutopata maambukizi ya Corona.

Pamoja na hayo Waziri Ummy amesema licha ya ugonjwa wa Corona kuelekea kumalizika nchini, amewataka wananchi kutobweteka na kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam wa afya ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kuvaa barakoa za vitambaa wanapokua kwenye mikusanyiko

Post a Comment

أحدث أقدم