Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imetenga kiasi cha shilingi 750 milioni kwa ajili ya kuwaendeleza washindi 70  wanaotokana mashindano ya ubunifu wa Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yaliyofanyika Machi 16 hadi Machi 20 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Waziri  wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako  wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ambapo amesema fedha hizo zitatumika kuwaendeleza wavunifu hao ili kazi zao ziwe kibiashara na kuwainua kiuchumi.

Aidha Prof. Ndalichako amesema kuwa Serikali itaendelea kutenga fedha zaidi mwaka hadi mwaka kwa ajili ya kuendeleza bunifu mbalimbali nchini.

“Natoa rai kwenu na washindi wote kuendeleza bunifu zenu ili kuhakikisha zinakuwa fursa za kiuchuni kwenu”, ametoa wito Prof. Ndalichako.

Prof. Ndalichako amesema,Serikali imetoa shilingi milioni 5 kwa washindi wa kwanza katika makundi yote ,shilingi milioni 3 kwa washindi wa pili kwa makubdi yote na shilingi milioni 2 kwa washindi wa tatu katika makundi yote.

Makundi yaliyoshiriki katika mshindano hayo ni pamoja na shule za msingi,  sekondari,vyuo vya ufundi stadium,vyuo vya ufundi wa kati,vyuo vikuu ,taasisi za utafiti na maendeleo pamoja na Mfumo usio rasmi.

Mashindano ya ubunifu wa Teknolojia (MAKISATU) hufanyika kila mwaka kwa wabunifu kutoka makundi mbalimbali kuonyesha ubunifu wao na hii ni katika kukuza teknolojia na kuibua vipaji hapa nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post