Kilichoibeba Tanzania, Uganda na Kenya kuandaa AFCON 2027 hiki hapa
Kenya, Uganda na Tanzania zitaandaa kwa pamoja fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) leo huko Cairo, Misri kutangaza kuwa ombi lao la pamoja limeshinda dhidi ya maombi ya Algeria, Misri na Botswana ambazo nazo ziliomba kuandaa fainali hizo.
Rais wa CAF, Dk Patrice Motsepe alitangaza rasmi ushindi wa maombi hayo ya nchi hizo tatu zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati ya utendaji ya shirikisho hilo ambacho wajumbe wake 22 walipiga kura ya kuchagua mshindi kati ya tenda nne zilizowasilishwa mezani.
"Kikao kilijikita zaidi katika kuangalia maslahi ya mpira wa miguu Afrika. Mchakato wa kumpata mwwenyeji wa fainali za 2027 ndio ulikuwa wa kuvutia zaidi lakini kiukweli kila nchi iliyoomba kuandaa fainali hizo, imeonyesha uwezo thabiti na utayari wa rasilimali na tunaona fahari katika hilo. Nitumie fursa hii kufkisha pongezi na shukrani zangu za dhati kwa marais wa nchi zote zilizotuma maombi.
"Hivyo nchi ambayo kamati ya utendaji imeichagua kuandaa Afcon 2027 ni Kenya, Uganda na Tanzania. Hii ni mara ya kwanza kwa muda mrefu sana, kwa Cecafa (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati) kuandaa fainali hizi. Na jambo la kuvutia ni kwamba wakati wa kuwasilisha, marais wa nchi zote tatu walionyesha utayari na uungaji mono wa kutimiza vigezo," alisema Motsepe.
Motsepe alisema kuwa kilichobeba maombi ya pamoja ya Tanzania, Kenya na Uganda mbali na utayari huo wa marais wa nchi husika ambao ni Samia Suluhu Hassan (Tanzania), Yoweri Museven (Uganda) na William Ruto wa Kenya ni urahisi wa usafiri wa watu kutoka eneo moja hadi lingine, uhakika wa miundombinu na pamoja na ukarimu wa watu wake.
Haikuwa rahisi
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro alifichua kwa gazeti hili kuwa walilazimika kufanya kazi ya ziada ili kushawishi wajumbe wa kamati ya utendaji ya CAF kuyapa ushindi maombi yao.
"Nawashukuru wote waliofanikisha ushindi huu. Nawashukuru vyama vya soka vya nchi hizi tatu. Lakini kubwa zaidi tunatoa shukrani kubwa kwa kamati ya utendaji ya Caf ambacho kimetuchagua. Mchakato haukuwa mwepesi na ulikuwa mgumu sana. Unapokuwa na nchi kama Algeria ambayo inaweza kuandaa Afcon wakati wowote, Senegal ambayo ina mafanikio makubwa kisoka, Nigeria ambayo inajua fitina za kimpira na Botswana inayoungwa mkono na nchi zote za Cosafa, ni lazima ufanye kazi ya ziada.
"Umoja wetu ulikuwa muhimu sana katika kuwezesha hili. Sasa baada ya kupata ushindi kinachofuata ni maandalizi ambayo tutahakikisha tunayafanya ya kiwango cha juu ili tuwe na fainali bora zaidi za Afcon kuliko zote zilizopita," alisema Dk Ndumbaro.
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha alisema kuwa ushindi huo ni hesima kubwa kwa Kenya, Uganda na Tanzania.
"Hili ni jambo kubwa sana ambalo limeletwa kwetu. Tunashukuru sana kwa watu wote waliotupa ushirikiano. Suala la vigezo na utayari wa serikali vimechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio haya," alisema Msitha
Algeria, Morocco wasaidia
Habari kutoka chanzo cha ndani ya CAF, kimelifichulia gazeti hili kuwa kitendo cha Algeria kujitoa katika dakika za mwisho kwenye mchakato huo kilichangia kwa kiasi kikubwa ushindi wa maombi ya pamoja ya Kenya, Uganda na Tanzania kuandaa Afcon 2027.
Baada ya Algeria kujitoa, nchi hiyo ilishawishi wajumbe ambao walikuwa wanaiunga mkono, kupiga kura zao kwa kuchagua maombi ya Tanzania, Kenya na Uganda badala ya kupigia kwa mataifa mengine yaliyoomba uenyeji wa fainali hizo.
Kibarua kizito kilibakia kwa turufu ya Morocco ambayo ina nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya kamati ya utendaji ya CAF ambapo ilitegemewa nchi watakayoiunga mkono iwe katika nafasi nzuri ya kushinda na inaripotiwa kuwa nayo ilishawishi wajumbe wake wachague maombi ya Tanzania, Kenya na Uganda kutokana na mahusiano mazuri waliyonayo na mataifa hayo.
Historia, rekodi yaandikwa
Kitendo cha maombi ya Tanzania, Kenya na Uganda kuchaguliwa kuandaa Afcon 2027 kimefanya kuandikwa kwa rekodi mpya ya fainali za Afcon kwa mara ya kwanza kuandaliwa na mataifa matatu kwa wakati mmoja ambapo hapo awali idadi kubwa ya nchi zilizowahi kuandaa kwa pamoja zilikuwa mbili tu.
Lakini pia historia mpya imeandikwa kwa nchi za Afrika Mashariki kuandaa fainali za Afcon kwani kabla ya hapo hakuna iliyowahi kufanya hivyo.
Fainali hizo za Afcon 2027 zitakuwa za sita kuandaliwa na nchi wanachama wa Cecafa ambapo mara tano zilizopita ziliwahi kuandaliwa katika nchi za Sudan na Ethiopia mwaka 1957, 1962, 1968, 1970 na 1976.
إرسال تعليق