Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amemaliza mgogoro uliodumu miaka 43 kati ya mmiliki wa eneo lenye ukubwa wa ekari 6. 8 sawa na mita za mraba 25,969 lililopo Makao Mapya kata ya Sinon katika jiji la Arusha Bibi Naasi Murio na wavamizi 110 ambapo imeamuriwa mmiliki huyo kulipwa jumla ya shilingi milioni 519, 380, 000 na Wavamizi hao.
Lukuvi amehitimisha mgogoro huo alipozungumza na wavamizi hao katika mkutano uliofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Sinon mkoani Arusha ambapo sasa bibi Murio atatakiwa kulipwa fedha hiyo katika kipindi cha miezi mitatu.
Alisema, uamuzi uliofanywa na serikali kuwataka wavamizi kumlipa Bibi Murio kiasi hicho cha fedha ni huruma kwa kuwa mahakama ilishatoa uamuzi kwa kumpa haki mmiliki na kilichotakiwa ni utekelezaji wa amri ya Mahakama ya kuondolewa wavamizi katika eneo hilo.
Aidha, Lukuvi alisema thamani ya kiwanja katika eneo hilo kwa sasa ni shilingi 50, 000 kwa mita ya mraba moja lakini kwa huruma ya serikali wavamizi hao watatakiwa kulipa 20, 000 kwa mita ya mraba jambo alilolieleza limelenga kuwahurumia wavamizi hao.
Kwa mujibu wa Lukuvi, wananchi waliovamia eneo hilo lenye nyumba za makazi, biashara pamoja na Kanisa wanatakiwa kumlipa bibi Murio kiasi cha pesa kulingana na ukubwa wa kila kiwanja cha mvamizi.
Hata hivyo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, pamoja na wavamizi kulipa kiasi hicho cha pesa watakiwa pia kulipa gharama nyingine kama vile fomu ya maombi ya kiwanja na gharama ya kutengenezewa Hati ya kumilikishwa kiwanja.
Post a Comment