Hivi leo vitabu ni moja kati ya vyanzo vikuu vya maarifa; ingawa bado watu wengi hawafahamu tunu inayopatikana katika vitabu.


Mara nyingi umekuwa ukisoma vitabu kadha wa kadha ambavyo vimekuburudisha au hata kukufundisha mambo mengi. Lakini pia inawezekana wewe una mambo ambayo ungependa kuyaweka katika vitabu.



Ni wazi kuwa kuna mbinu mbalimbali unazoweza kuzitumia kuandika kitabu ili kiweze kufikisha ujumbe au kutimiza lengo lililokusudiwa. Karibu ufahamu mbinu  zitakazokuwezesha katika uandishi wa vitabu.



1. Chagua wazo bora
Hatua ya kwanza kabisa katika uandishi wa kitabu ni kuchagua mada au wazo bora. Hakikisha unachagua wazo au mada kwa makini ambayo itakuwezesha kukamilisha lengo lako. Unaweza kuzingatia haya:
Chagua mada ambayo unaipenda na unaielewa vyema.
Chagua mada ambayo inahitajiwa na wasomaji.
Chagua mada ambayo haikiuki sheria au maadili ya eneo unalolenga.
Chagua mada ambayo inaziba pengo lililoachwa na vitabu vingine.



2. Pangilia kabla ya kuandika
Mpangilio ni jambo muhimu sana katika uandishi wa vitabu. Hakikisha unapangilia mtiririko wa mawazo pamoja na muundo mzima wa kitabu chako kabla ya kuanza kuandika. Hakikisha unabainisha sura zitakazokuwepo kwenye kitabu chako pamoja na kitakachozungumziwa katika sura hizo.



Ikiwa unashindwa kupanga mawazo pamoja na kubainisha sehemu kuu za kitabu chako, basi kuna haja ya kutafakari upya wazo ulilolichagua.



3. Zingatia kanuni za uandishi
Uandishi ni taaluma kamili; hivyo ni muhimu kuzingatia kanuni bora za uandishi kama vile matumizi bora ya lugha, mpangilio wa hoja au mawazo pamoja na matumizi ya alama za uandishi. Ikiwa wewe siyo mtaalamu mzuri wa lugha; unaweza kutafuta mtaalamu wa lugha anayeweza kukusaidia kuboresha kazi yako.



4. Zingatia mazingira bora ya uandishi
Siyo kila mazingira yanafaa kwa ajili ya kufanya kazi ya uandishi; ni lazima uhakikishe unatafuta mazingira ambayo ni tulivu na yasiyokuwa na muingiliano. Katika swala la kuandaa mazingira unaweza kufanya haya yafuatayo:



Tafuta eneo lililotulia lisilo na usumbufu wowote.
Tenga muda ambao uko vizuri kiafya na kiakili. Mara nyingi muda wa asubuhi ni bora zaidi kufanya kazi hii kwani mwili na akili vinakuwa viko vizuri.



Ondoa vitu vinavyoweza kukuvuruga kama vile mitandao ya kijamiii, televisheni, simu, watu wasiohusika, n.k.



Kwa kufanya hivi utaweza kupata utulivu wa kutosha na kuweza kuondoa vitu ambavyo vinaweza kuingilia shughuli yako ya uandishi.



5. Tafuta kazi inayoshabihiana
Mara nyingi kila kitu duniani kina kitu kingine kinachoshabihiana nacho. Tafuta kitabu ambacho kinakaribiana na kile unachotaka kuandika; kwa kufanya hivi utaweza kukitumia kama mwongozo wako.



Tazama jinsi ambavyo mwandishi wa kitabu husika amepanga mawazo au hoja katika kitabu chake; tazama pia lugha na mbinu nyingine za kiuandishi alizozitumia kukamilisha kazi yake.



6. Tambua hadhira
Aina za uandishi hutofautiana baina ya aina moja ya hadhira na nyingine. Uandishi wa vitabu vya watoto ni tofauti na uandishi wa vitabu vya vijana au wazee. Hivyo ni muhimu ukabaini ni kundi gani na lenye sifa gani unalolilenga katika kitabu chako. Ifahamu vyema hadhira yako, fahamu inapendelea nini ili uweze kuilenga vyema.



7. Zingatia uhariri
Hakuna uandishi bora pasipo uhariri bora. Ni muhimu sana ukazingatia uhariri kwani utakuwezesha kufanya kazi bora ambayo itaonekana imefanywa kitaalamu. Hakikisha unapata muda wa kutosha wa kuhariri hoja, mawazo, mpangilio pamoja na lugha katika kitabu chako.



Ikiwa huna uwezo au muda wa kuhariri kitabu chako basi unaweza kutafuta mhariri akakusaidia kuhariri kitabu chako.



Uandishi wa vitabu ni taaluma pana ambayo inahitaji uzoefu wa muda mrefu ili kuimudu vyema. Lakini kama utafanya maamuzi ya dhati ya kuzingatia mbinu hizi za uandishi wa vitabu, ni wazi kuwa utaweza kumudu swala la uandishi wa vitabu ndani ya muda mfupi. Usisubiri, anza kuandika leo, ndipo utakapozidi kukomaa kadri siku zinavyosogea.

Post a Comment

Previous Post Next Post