Robert Gabriel Mugabe alizaliwa mnamoo tarehe 21 Februari 1924 na kufariki 6 Septemba 2019. Robert Mugabe alikuwa kiongozi mkuu wa Zimbabwe tangu 1980 hadi 2017., ambapo alikuwa mwenyekiti wa chama tawala cha ZANU cha nchini zimbabwe.
Mwaka 1980 alikuwa waziri mkuu na mwaka 1987 Rais wa Zimbabwe. Kabla ya wakati ule aliongoza upinzani wa ZANU dhidi ya serikali ya walowezi Waingereza nchini waliofuata siasa ya ubaguzi wa rangi.
Mugabe alirudia kushinda katika uchaguzi mara kadhaa. Tangu mwaka 2000 chaguzi hizo zilitiwa shaka kutokana na matishio na matumizi ya mabavu dhidi ya wapinzani. Utawala wa Mugabe umeitwa wa kidikteta tangu mwaka 2002. Kutokana na mashtaka dhidi ya serikali ya Mugabe ya kudharau haki za binadamu, nchi ya Zimbabwe ilisimamishwa ndani ya Jumuiya ya Madola. Mugabe pamoja na mawaziri wake na viongozi wa chama chake hawakuruhusiwa kusafiri kwenda nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani.
Mwanzoni mwa utawala wake Mugabe alisifiwa kujenga uchumi na sera ya elimu nchini. Zimbabwe ilikuwa nchi iliyouza chakula kwa wingi nje. Tangu mwanzo wa milenia mpya pamoja na mashtaka ya udikteta hali ya uchumi ilirudi nyuma. Takriban raia milioni mbili wa Zimbabwe wameondoka nchini wakakaa kama wakimbizi Afrika Kusini.
إرسال تعليق