Mtu wa kwanza anayekuzuia kufanikiwa ni wewe mwenyewe; sio jamii, siyo serikali au mtu mwingine yeyote katika maisha yako. Ni kweli kuwa baadhi ya watu huanza maisha katika mazingira rafiki zaidi, lakini ninaamini kila mmoja ana nafasi na uwezo ya kufanikiwa.
Haya ni baadhi mambo ambayo watu wengi wamekuwa wakiyafanya na kujiambia na yamewatenga na mafanikio yao.
Ninahitaji shahada ya chuo kikuu ili kufanikiwa
Unahitaji shahada kupata kazi katika ofisi fulani lakini si kuwa majasiriamali katika ofisi yako wewe mwenyewe.
Ipo mifano kadha wa kadha duniani ya watu waliofanikiwa na kuwa mabilionea wakubwa bila kuwa na shahada ya chuo kikuu. Mfano wa watu hao ni Mwanzilishi na mmiliki wa mtandao wa Facebook Mark Zuckerberg. Hivyo basi fanya maamuzi leo ili ufikie kiwango bora cha maisha kwani kizuizi pekee ni wewe.
Sina muda wa kutosha
Hili ni swala ambalo watu wengi hulalamikia kila siku kuwa hawana muda kutosha. Fahamu kuwa hakuna binadamu duniani mwenye zaidi ya saa 24. Hivyo kama unapata muda wa kutumia mitandao ya kijamii, kucheza michezo ya kompyuta au kuchati kwa simu basi una muda mwingi mno kuliko unavyofikiri.
Badilisha fikra zako leo, jifunze kutumia muda wako vyema ukijiwekea vipaumbele na malengo ya kukamilisha kila siku.
Umri wangu umeenda sana
“Haujachelewa kuwa ambaye ungeweza kuwa.”
George Eliot
Watu wengi wamekuwa wakihofia swala la umri, hasa pale wanapotazama na kuona kuwa hawapo kwenye miaka kati ya 20 hadi 30. Lakini ukweli ni kwamba umri sio kizuizi bali fikra zako ndiyo kizuizi.
Usikubali kuacha ndoto na malengo yako yafifie gizani. Amka!, amka sasa na ufanye maamuzi tekelevu juu ya maono na mipango yako.
Ni vigumu kuanza
Ni kweli kuwa hata wahenga walisema “mwanzo ni mgumu” lakini hilo sio kanuni. Kila mtu duniani angewaza mwanzo ni mgumu nafikiri tungekuwa bado kwenye zama za ujima.
Jifunze kwa waliofanikiwa, walianzaje? walizikabili vipi changamoto? Siku zote jifunze kuona mafanikio kabla ya changamoto, hili litakupa hamasa na kiu ya kufanya bidii hata kuzishinda changamoto.
Inasikitisha kuona kuwa watu wengi hawafikii malengo yao kwa sababu ya mambo wanayojiambia au kujiwazia wenyewe. Ninakuhamasisha kuwa, kama unapumua basi unaweza kufanikiwa. Inaweza kuchukua muda lakini ukiamua unaweza
إرسال تعليق