SALVATORY NTANDU
Ukosefu wa huduma ya Maji safi na Salama kwa Wakazi kata ya Ngogwa katika Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga umetajwa kuhatarisha Maisha ya  wanawake  kutokana na baadhi yao kujeruhiwa na wanyama aina ya fisi pindi wanapokwenda kuchota maji kwenye visima vilivyopo umbali wa kilomita 6 nyakati za alfajiri.

Kauli hiyo imetolewa June 5 Mwaka huu na Diwani wa Kata ya Ngogwa,Kamuli Mayunga wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kahama iliyotembelea Mradi wa Maji Safu wa Ngogwa-Kitwana unaojengwa na Mamlaka za Maji, SHUWASA, KUWASA na RUWASA.

Alisema kuwa Kumekuwa na Matukio mengi ya wanawake kushambuliwa na wanyama hao ambao wanapatikana kwa wingi katika eneo hilo kutokana na kuwepo kwa milima mingi na kusema kuwa kukamilika kwa mradi huo utaweza kutokomeza matukio hayo sambamba na magonjwa ya homa za matumbo.

“Tunashukuru ujio wa Mradi huu miaka miwili iliyopita tulipoteza wanawake wawili kwa kushambuliwa na fisi hadi kufariki dunia wakati wakienda kuchota Maji nyakati za alfajiri,Tunaipongeza serikali kwa kusikiliza kero hii ya kumtua mama ndoo kichwani,”alisema Kamuli.

Celina Paulo ni Mkazi wa kijiji cha Nyamela alisema kuwa fisi wamekuwa kikwazo kwao pindi wanapokwenda kuchota Maji asubuhi na kuiomba Serikali kuhakikisha wanakamilisha Mradi huo kwa wakati ili kuwaondolea adha hiyo ili kundelea na shughuli zingine za uzalishaji Mali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) Flaviana Kifizi alisema Mradi huo umekamilika kwa asilimia 95 na utagharimu shilingi bilioni 2.4 na utakamilika mwezi Agosti Mwaka huu na unatarajia kunufaisha zaidi ya wakazi 1000 wanaoishi pembezoni mwa Halmashauri hiyo.

“Ujenzi wa Matanki Mawili ya Ngogwa na Kitwana umekamilika na kwa sasa tunatarajia kuanza kulaza mabombo ili kuruhusu maji kuanza kutumiwa na wananchi,pia tutajenga vituo 13 vya kuchotea maji ambayo yatawawezesha wananchi kupata huduma za maji safi na salama ambayo itakuwa suluhisho la wao kutembea umbali Mrefu kutafuta huduma hiyo,”alisema Kifizi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya ya Kahama,ambaye ndio Mkuu wa wilaya hiyo Anamringi Macha alisema kuwa serikali ya awamu ya Tano Chini ya Dk John Pombe Magufuli imedhamiria kitatua kero zote za wananchi hususani ya Maji kwa kuhakikisha wanapata maji safi na salama.

“Katika mradi huu niwaombe wananchi msiweke vikwazo pindi watakapoanza kuchimba mitaro ya kupitisha Mabomba kwani hakuna mtu atakayelipwa fidia,tutoe ushirikiano ili kufanikisha mradi huu kwa wakati na tuendelee na shughuli za uzalishaji maji kupita huduma ya maji,”alisema Macha.

Post a Comment

أحدث أقدم