NA FAKI A. FAKI
Waswahili walisema usichokijua ni kama usiku wa kiza, tena kile kiza kinene. Chembe ndogo tu ya shari inaweza kuuharibu utamu wote wa maisha ukatamani ardhi ipasuke uingie ndani mambo yaishe. Lakini hujui huko ardhini nako kuna madhila gani. Pengine unaweza kukutana na madhila makubwa zaidi kuliko uliyoyakimbia duniani.
Nilipoanza kazi ya upolisi hakukuwa na kitu kilichonifurahisha kama kazi ya upelelezi. Nilifurahia sana kupeleleza kadhia mbalimbali hasa zile za makosa ya jinai.
Nilifurahia sana kuwahoji watuhumiwa na kuwabana kwa maswali na wakati mwingine kutishia kuwaweka ndani hasa pale ninaposhuku kuwa wanachonieleza ni uongo.
Lakini siku moja tu niligundua hakuna kitu kibaya kama kuwa mtuhumiwa na kuwa mbele ya afisa wa polisi kama mimi ukihojiwa maswali.
Niligundua hivyo siku ile kibao kiliponigeukia mimi na kujikuta nipo mbele ya afisa wa polisi tena mwanamke niliyemzidi kiumri.
Nilijisikia vibaya hasa alivyonibainishia kuwa maelezo niliyompa yalikuwa ya uongo ambayo niliyatoa kuficha ukweli….
Hapo ndipo kitanzi nilipokiona waziwazi machoni mwangu. Kilikuwa kinasubiri saa tu….
SASA ENDELEA
Jina langu ni Fadhal Amrani Bwanga. Ni mzaliwa wa Morogoro.Elimu ya msingi nilisomea Morogoro. Elimu ya sekondari pamoja na chuo kikuu niliipata Dar es salaam.
Aliyenigharamia elimu yangu ya sekondari hadi kidato cha sita ni babu yangu mzee Bwanga ambaye alikuwa akiishi Dar es Salaam.
Wakati namaliza darasa la saba, shule ya msingi, baba yangu mzee Amrani Bwanga alifariki dunia.
Yeye alikuwa dereva wa malori. Alipata safari ya kwenda Kongo. Baada ya mwezi mmoja tukapata taarifa kuwa lori alilokuwa akiendesha limetekwa nyara na kundi la waasi.
Baada ya wanajeshi wa vikosi vya serikali kufuatilia waligundua kuwa mzee Amrani aliuawa pamoja na otingo wake. Miili yao ilikutwa imetupwa msituni. Baba yangu alikutwa na majeraha ya risasi mbili. Risasi moja alipigwa kifuani na nyingine alipigwa kichwani.
Miili yao ililetwa Dar es Salaam kwa mazishi. Baada ya kutua Dar es Salaam ikasafirishwa Morogoro. Ndipo babu yangu alipochukua jukumu la masomo yangu.
Baada ya kupata digrii yangu ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mlimani jijini Dar es Salaam, nilipata ajira katika jeshi la polisi.
Kwa sababu tayari nilikuwa msomi wa chuo kikuu, masomo yangu katika jeshi hilo yalikuwa ya uofisa. Nilianza kazi nikiwa na nyota moja.
Kituo changu cha kazi cha kwanza kilikuwa Tanga ambako nilifanya kazi katika kituo cha polisi cha Ngamiani. Wakati naanza kazi, kituo hicho kilikuwa bado kipya na nilimkuta mkuu wa kituo mwenye nyota tatu ambaye elimu yake ilikuwa ya sekondari. Alipanda vyeo kwa sababu ya utumishi wa muda mrefu.
Baadhi ya marafiki zangu walinilaumu kuongozwa na mtu ambaye nilimzidi kielimu. Niliwaambia huo ndio utaratibu wa kazi unaozingatia sifa ya kazi ikiwemo uzoefu na kutumika kwa muda mrefu.
Hata hivyo niliifurahia kazi yangu kwa vile katika kituo hicho maafisa walionizidi kicheo walikuwa wawili. Alikuwa mkuu wa kituo mwenye nyota tatu. Msaidizi wake mwenye nyota mbili na mimi ambaye nilikuwa na nyota moja.
Msaidizi wa mkuu wa kituo alikuwa mwanamke ambaye kiumri tulikuwa kama tunalingana sema yeye alianza kazi kabla yangu. Alinitangulia kwa karibu miaka mitano.
Kuchelewa kuanza masomo ya msingi, kurudishwa darasa mara kwa mara na miaka niliyoitumia kuchukua digrii yangu, ndivyo vitu vilivyonichelewesha sana.
Nyuma ya kituo kulikuwa na nyumba kadhaa za polisi ikiwemo nyumba niliyokuwa nikiishi mimi. Baada ya kazi sikuwa nikisumbuka kwenda mbali, nilikuwa nikitembea kwa miguu umbali mfupi tu kurudi nyumbani.
Kazi hii ya upolisi sikuwa nimeipata kibahati bahati. Ilikuwa ni miongoni mwa kazi ambazo nilikuwa na ndoto nazo. Kazi ya kwanza niliyoitaka ilikuwa ni ya uhakimu. Kazi ya pili uhariri wa vyombo vya habari na kazi ya tatu ni ya upolisi.
Kwa vile nafasi zilikuwa haba katika vyombo vya habari na katika uhakimu, nikaamua kujiunga na jeshi la polisi kwa vile wakati ule namaliza masomo yangu chuo kikuu, zilitokea nafasi za kazi katika jeshi hilo.
Nilikuwa nafurahia sana kupeleleza kesi kuliko nilivyofurahia kupambana na majambazi. Nilikuwa hodari sana kuwahoji maswali washukiwa, kuwachunguza na hatimaye kumpata mhalifu.
Nilikuwa na vitisho vya kuwaweka washukiwa mahabusi, wakati mwingine kuwacharanga makofi na pia kutumia sana ile lugha ya kumpeleka mtu mahakamani.
Na kwa kweli tangu nilipoanza kazi yangu nilishawachunguza washukiwa wengi, kuwaweka ndani na wengine kuwapeleka mahakamani. Katika watuhumiwa niliowachunguza na kuwafikisha mahakamani hakukuwa na yeyote aliyesalimika. Wote walipatikana na hatia na kukabiliwa na vifungo au faini.
Hii ikaniongezea sifa katika kazi yangu kwa kuonekana nilikuwa polisi hodari niliyekuwa nikiitumia vizuri elimu yangu katika kazi yangu.
Uhodari wa polisi ni kuzuia uhalifu kwa namna yoyote ile, kukamata, kushuku kosa na kuhakikisha watuhumiwa unaowafikisha mahakamani wanapatikana na hatia.
Hii ni sifa nzuri kwa polisi lakini si sifa nzuri kwa baadhi ya raia. Polisi wa aina hii mitaani anaonekana mchungu kuliko mwarobaini. Watu humlaani na kumuapiza kila anapopita.
Lakini nilichokuwa ninakijali mimi si kuchukiwa na watu wenye nia mbaya bali kutimiza jukumu langu la kulinda amani na usalama wa raia kama polisi mwaminifu ninayechukia rushwa na fitina.
Lakini siku moja ambayo sitaisahau maishani mwangu nilikuwa na zamu ya kuingia usiku kazini kwangu. Usiku huo tulikuwa maafisa wawili kwenye kituo hicho. Mimi na mkuu wa kituo msaidizi.
Kwa kawaida afisa akiingia katika zamu ya usiku anakuwa mmoja tu lakini usiku huo tulikuwa maafisa wawili kwa sababu maalumu. Polisi wengi walikuwa wamepelekwa katika kitongoji cha Amboni kilichokuwa kilometa chache kutoka jiji hapo.
Polisi hao walipelekwa baada ya kupatikana kwa taarifa kwamba kikundi cha magaidi wa kundi la Al shabab kimejichimbia katika kitongoji hicho kwa nia ya kufanya shambulio.
Katika kituo hicho tulibaki polisi wanne tu akiwemo afisa wangu ambaye alikuwa akipokea taarifa kwa radio call zilizotoka huko Amboni.
Mimi pamoja na polisi wawili tulikuwa kaunta tukihudumia wananchi waliofika hapo kwa shida mbalimbali.
Baada ya kuchoka kukaa kwa muda mrefu nilitoka na kuanza kuranda randa mbele ya lango la kituo. Mara kwa mara nilikuwa natazama saa yangu. Yalikuwa majira ya saa saba na nusu usiku nilipoona teksi ikisimama mbele ya kituo hicho. Nyuma ya teksi niliona pikipiki iliyopita mbio na kuendelea na safari.
Nilikuwa nikiitazama ile teksi kuona nani atashuka. Punde tu nikamuona msichana mmoja aliyekuwa amevaa baibui la kisasa mfano wa joho. Kichwani alikuwa amefunga kilemba cha kike cha kitambaa cha rangi ya samli ambayo ilikuwa rangi ya lile baibui alilovaa.
Alikuwa mweupe mwenye sura na umbile la kupendeza. Alikuwa ameshika mkoba wa ngozi ambao ulikuwa wa rangi ileile ya samli.
Wakati teksi inaondoka alitembea kuelekea kwenye lango la kituo hicho huku uso wake ukionesha kufadhaika.
Akakutana na mimi niliyekuwa nikivinjari mbele ya lango.
Alinitazama usoni kwangu kisha akanisalimia.
“Habari ya kazi?”
“Nzuri” nikamjibu huku nikimtazama kwa makini kabla ya kumuuliza.
“Una shida gani?”
“Nina shida na ninaomba msaada wenu”
“Ndiyo ueleze ni shida gani?’
“Mimi natoka Dar ninakwenda Mombasa. Nilitegemea kufika hapa saa tatu usiku ili nipande basi linaloondoka saa nne usiku kwenda Mombasa lakini basi nililopanda liliharibika mara mbili. Badala ya kufika hapa saa nne lilifika hapa saa tano na nusu. Basi la kwenda Mombasa lilikuwa limeshaondoka”
“Kwa hiyo?”
“Sina mwenyeji hapa Tanga. Dereva wa teksi alinipeleka katika gesti zaidi tano, zote zimejaa wageni. Nimeambiwa kuna mkutano wa kitaifa chama fulani unafanyika hapa Tanga kesho, hivyo gesti nyingi zitakuwa zimejaa. Lakini nilikuwa na wasiwasi na pikipiki ambayo ilikuwa ikinifuatilia nyuma muda wote nikiwa kwenye teksi”
Msichana huyo aliendelea kunieleza.
“Sikuweza kufahamu watu hao wenye pikipiki walikuwa kina nani, walikuwa watu wabaya au wazuri. Dereva wa teksi akanishauri nisiendelee kutafuta gesti bali anilete hapa kituo cha polisi niombe msaada wa kujihifadhi hadi kesho asubuhi ambapo nitapanda basi la saa moja asubuhi niende Mombasa”
Wakati wote akinieleza maneno yake, nilikuwa namtazama kuanzia kichwani hadi miguuni. Haidhuru ilikuwa tabia ya kipolisi kumkagua mtu anayezungumza naye ili kumsoma na kumuelewa kama maelezo anayotoa yalikuwa ya kweli au la. Kumtazama kwangu kulikuwa nje ya sababu za kipolisi.
Yule msichana alikuwa amevaa cheni niliyohisi ni ya dhahabu, bangili za dhahabu na vipuli vya dhahabu. Haidhuru sikuwa nimesimama naye kwa karibu sana, nilikuwa nikisikia hewa ya manukato murua iliyokuwa ikitoka mwilini mwake.
Lakini mbali ya hayo, sauti yake ilikuwa laini na alikuwa akizungumza kwa lafudhi ya Kiswahili cha kipwani.
Wakati namtazama nilikuwa najaribu kumtambua alikuwa msichana wa wapi, Zanzibar, Bagamoyo, Pangani au Mombasa alikosema alikuwa anataka kwenda.
Lakini bado kuna kitu kimoja ambacho hujitokeza mwanaume anapozungumza na msichana, kumchunguza kwa macho kuona kama alikuwa amependeza.
Yule msichana alikuwa amependeza na kwa kweli alinitamanisha. Wakati wote alipokuwa akinitolea maelezo yake moyo wangu ulikuwa umeshaingia kwenye mahaba.
Itaendelea….
Post a Comment