Kwa jinsi maisha yanavyokwenda kasi hususani utandawazi hakuna shaka yoyote kuwa mtu uppo radhi hata ugharamie pesa ili uchaji simu yako, hii yote usipitwe na habari, au dili nyingine ambazo kwa maisha ya sasa zinakamilishwa kupitia simu.
Nakumbuka mwaka jana nilifanya tafiti ndogo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya UDSM, UDOM na SAUT kuhusu maisha bila simu inawezekana? Asilimia 90% kati ya wanafunzi 120 walisema hawawezi kuishi bila simu wala kukaa mbali na simu zao, huku asilimia 10% tu ndiyo walisema wanaweza kuishi bila simu.
Hii ni ishara kuwa kwa ulimwengu wa sasa kama hauna simu huenda ukawa upo nyuma ya ulimwengu wa Teknolojia kwani vitu karibia vyote vinakamilishwa kupitia simu.
Je, changamoto gani ambayo inaumiza sana au inaboa watu wengi kwenye matumizi ya Simu? zipo changamoto nyingi kama ukosefu wa vocha lakini kubwa zaidi ni Changamoto ya CHAJI.
Nadhani hili ni tatizo kubwa sana kwani kwenye mikusanyiko mikubwa siku hizi kama kwenye sherehe au mikutano sio jambo la kushangaza kumuona mtu akikuomba Charger pengine hata kama hamjuani.
Je, tatizo nini mpaka kuwe na usugu wa tatizo hilo? jibu ni kwamba watumiaji wengi wa simu za mikononi hawasomi maelekezo ya jinsi ya kutunza betri za simu zao na kuishia kulalama kuwa betri zao ni FEKI.
Basi nakuhakikishia kuwa betri ya simu yako sio feki wala mbovu ila hujui jinsi ya kutunza Betri yako, Kwahiyo kama betri yako inakusumbua kwenye chaji usiamini kuwa betri yako ni FEKI fuatilia hatua hizi wakati wa kuchaji simu ili simu yako iweze kuhifadhi chaji muda mrefu.
1-Epuka kuchaji Simu mara kwa mara kwa kutumia kihifadhi Chaji (Power Bank).
Kumekuwa na kesi nyingi za watu kulalamika mara baada ya kutumia Power Bank wengi wao wakisema simu zao hazitunzi chaji, ukweli ni kwamba Power Bank huhifadhi chaji kama betri la simu lilivyo hivyo kitendo cha kuchaji betri lingine husababisha maambukizi ya mtiririko wa Chaji hivyo hufanya betri kupoteza nguvu ya kuhifadhi chaji kadri unavyozidi kutumia mara kwa mara.Hapa unashauriwa kutumia umeme wa moja kwa moja kutoka kwenye Soketi wakati wa kuchaji na sio vihifadhi chaji.
2-Epuka kutumia Program (App) zenye matangazo mengi.
Nadhani ushawahi kuliona hili kama ni mtumiaji mzuri wa App mbalimbali hususani zenye matangazo mengi wakati wa kutumia huwa simu inashika joto haraka sana, Ukweli ni kwamba kwenye majaribio mbalimbali yaliyofanywa na wataalamu wa mitandao yamebaini kuwa programu zenye matangazo mengi huchukua karibia asilimia 30% ya chaji pindi unapozitumia pata picha una App tano zenye matangazo ni kiasi gani cha chaji utapoteza kwa wakati unatumia? bila shaka umepata jawabu. Hapa unashauriwa kutoa kabisa kama sio kupunguza matumizi ya Program hizo.
3-Epuka kutumia ‘Charger’ tofauti tofauti,(Tumia charger sahihi).
Kutokana na kukosa uelewa wa kusoma maelekezo kumekuwa na desturi kwa watu wengi siku hizi kugongea charger hususani maofisini au hata kwenye maeneo mengine ya kazi basi usifanye hivyo tena.
Kila simu ukisoma kwenye betri yake kuna maelekezo yameandikwa kwa nyuma kuwa usitumie Charger nyingine mbali na ile uliyopewa na simu, hii maana yake ni nini? ni kwamba Charger zinakuwa na Voltage yake inayopita kuchaji simu na hii hutofautiana sana kutokana na ukubwa na aina ya simu kwa hiyo kama simu yako inapitisha mfano Voltage 0.05 na ukatumia Charger inayopitisha voltage 0.5 lazima uharibu betri yako hivyo ni vyema ukajua charger ya simu yako inapitisha kiasi gani cha umeme kabla ya kutumia charger nyingine.
4-Epuka kuchaji simu au kuweka simu kwenye mazingira ya joto kali au baridi kali.
Simu nyingi hususani zile za kisasa haushauriwi kuziweka kwenye mazingira ya joto kali zaidi ya Celsius 50 kwani kwa kufanya hivyo kutafanya betri ya simu yako kupungua nguvu na hii pia ipo hata wakati wa kuchaji simu kama una tabia ya kuchaji simu ikiwa juani au sehemu yenye joto kali utaifanya simu yako ijae upesi lakini pia itawahi kuishana muda mwingine simu kulipuka au Betri kuvimba.
5-Chaji simu yako pale inapofikia asilimia kuanzia 16% hadi 10%.
Hapa wataalamu wengi wa masuala ya kielekroniki wanasema chaji simu yako pale tuu inavyoanza kulia mlio wa kuashiria betri yako inahitaji kuchajiwa.
Kwa bahati mbaya sana wameshauri kupunguza kabisa kama sio kuacha tabia ya kusubiri mpaka simu izime chaji ndiyo uanze kuchaji kwani kwa kufanya hivyo kutaathiri ions ambazo huhifadhi chaji na kwa muda mfupi sana utaona betri yako ikishindwa kuhifadhi kabisa chaji.
Ushauri kama utakuwa upo mbali na sehemu ya kuchaji simu yako na tayari imeshafika asilimia kati ya 10%-16% basi ni bora ukazima simu kabisa.
6-Kushindwa kuchaji simu vizuri na kwa ufasaha.
Hii ni sababu kubwa na mbaya sana hususani kwa watumiaji wa Smartphone huwa ni wanashindwa kustahimili muda wa kuchaji hujikuta wanachaji simu huku wakitumia au kuitoa simu chaji hata kabla ya kujaa hilo ni kosa kubwa sana.
Unashauriwa uchaji simu yako bila kuitumia mpaka betri ijae yaani (Full Charge) kwa kufanya hivyo utaiongezea betri uwezo wa kutunza chaji tofauti na mfumo wa kuchaji bila mpangilio maalumu.
Kuna kesi kibao za vifo ambavyo vimetokana na simu kulipuka kutokana na kutumia simu huku ikiwa kwenye chaji.
7-Epuka kuchaji simu ikiwa hewani (Zima au weka Flight Mode).
Jitahidi unapochaji simu yako kuizima au kuweka flight mode ni vizuri zaidi kama ungeweza kuweka flight mode kwa kuwa simu inajaa chaji vizuri ikiwa imewaka lakini haitumiki.
8-Hakikisha betri la simu yako limekaa vizuri kwenye simu.
Hii ni kwa watu wangu wanaotumia simu ndogo za au zile zenye uwezo wa kutoa betri hakikisha betri ya simu yako imebana vizuri kwenye koili za chaji za simu yako kwani kuna kiwango kikubwa cha chaji kinapotea kama simu yako imelega lega au kushikana vizuri na koili zinazotumika kuchaji simu yako.
Endapo utazingatia haya hakuna shaka yoyote uhai wa betri yako ya simu utaendelea kudumu na hautopata kamwe buguza za chaji kukata kata au kutembea na Power Bank kila sehemu.
إرسال تعليق