Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya Taifa ya kuogele ya waogeleaji chipukizi (Junior), Dennis Mhini ameng’ara katika mashindano ya Dunia yanayoendelea mjini Budapest, Hungary baada ya kuongoza katika kundi la kwanza mchujo.
Dennis ambaye ni mwanafunzi wa shule ya St Felix ya Uingereza, aling’ara katika shindano ya mita 100 katika mtindo wa Backstroke kwa kutumia muda wa 1.04,27 na kuwashinda waogeleaji wengine kutoka mataifa mbalimbali katika kundi la kwanza.
Aliweza kuwapita waogeleaji kutoka nchi za Albania ambayo iliongozwa na Ared Ruci, Madagascar iliyowakilishwa na Mandresy Rajaonson na Nigeria iliyokuwa chini ya muogeleaji, Adewole Adekoya.
Katika kundi hilo pia Dennis aliwachapa waogeleaji, Humza Khaliq wa Pakistan, Tsitocina Razanatefy (Madagascar), Amar Altub ali Altub wa Sudani na Mtanzania mwenzake, Isam Sepetu.
Matokeo ya kuongoza katika hatua ya mchujo yametoa faraja kwa Tanzania katika kuendeleza mchezo huo pamoja na changamoto ya kukosa bwawa la kuogelea la kisasa la mchezo huo.
Waogeleaji wa Tanzania wamekuwa na kilio cha kupata bwawa la mita 50 la kisasa kwa kipindi kirefu na kushindwa kuzoea vifaa vya kisasa.
Mabwawa mengi ambayo yanamilikiwa na taasisi binafsi (zaidi shule za kimataifa) yana urefu wa mita 25 na kukosa vifaa vya kisasa kama ‘diving block’ (kifaa kinachutumiwa na waogeaji kuchupa) na touchpad ambayo inatumika kwa ajili ya kurekodi muda.
“Nimefurahi kuongoza katika ‘heat’ yangu na kuitangaza nchi. Ni kazi kubwa sana kufikia hatua hii, kwangu mimi ni historian a hasa ukizingatia kuwa tunafanya mazoezi kwenye mabwawa ambayo hayalingani na haya ya kisasa na kulazimika kuja mapema Hungary ili kupata fursa ya kutumia mabwawa haya japo kwa siku mbili,” alisema Dennis.
Dennis Mhini akipozi mara baada ya kuibuka wa kwanza katika kundi la mchujo la kwanza (heat 1) katika mashindano ya Dunia ya Vijana yanayofanyika mjini Budapest, Hungary.
Muogeleaji wa Tanzania, Dennis Mhini akimaliza kwa kishindo na kuibuka wa kwanza katika kundi la mchujo la kwanza (heat 1) katika mashindano ya Dunia ya Vijana yanayofanyika mjini Budapest, Hungary.
Post a Comment