Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa orodha ya tatu ya majina ya wanafunzi waliopata mkopo yenye jumla ya wanafunzi 4785 wa mwaka wa kwanza wa masomo 2019/2020.
Wanafunzi hao wamepata mikopo yenye thamani ya Sh14.3 bilioni na hivyo kufanya idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo kufikia 46,838. yenye thamani ya sh162.86.
Taarifa iliyotolewa Jumapili Novemba 3, 2019 na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru imeeleza kuwa wanafunzi waliopata mikopo katika awamu ya tatu wanaweza kupata taarifa zao kupitia akaunti walizotumia kuomba mkopo
Badru amesema majina yote ya waombaji waliofanikiwa kupangiwa mikopo katika awamu hii yanapatikana katika mtandao wa HESLB wa uombaji mkopo (https://olas.heslb.go.tz)
Kuhusu taratibu za malipo kwa wanafunzi, amesema fedha za wanafunzi waliopata mikopo zimeshapelekwa vyuoni na vyuo vimeelekezwa kuhakikisha fedha zinawafikia wanafunzi walengwa mara wanapofika na kukamilisha taratibu za usajili.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga Sh450 bilioni kwa ajili ya wanafunzi 128,285. Kati yao, wanafunzi 83,285 ni wenye mikopo wanaoendelea na masomo ya mwaka wa pili, tatu na kuendelea.
Post a Comment