WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na
Rais Dkt. John Pombe Magufuli itahakikisha mali zote za wakulima wa zao
la mkonge nchini zinarudishwa mikononi mwao na hakuna mtu yeyote
atakayeonewa.
“Tutarudisha
mali zote za wakulima na ninawahakikishia hakuna mtu yoyote
atakayeonewa, kama tulivyorudisha hizi mali za Bodi ya Mkonge Tanzania
tutafanya hivyo hivyo kote bila kumuonea yeyote na kuanzia leo Bodi hii
ya Mkonge imethibitishwa kuwa bodi kamili.”
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Juni 1, 2020) wakati akifungua
jingo la Bodi ya Mkonge Tanzania zilizopo jijini Tanga. “Mkonge ni fedha
Halmashauri wekeni vitalu mzalishe mbegu muwape wananchi bure. Kama
unashamba kubwa hujaliendeleza, kulingana na muda uliowekwa,
tutalichukua.”
Amesema
Serikali imedhamiria kulirudisha zao hilo, hivyo ametoa wito kwa
wananchi hususani wa mkoa wa Tanga wajipange katika kuyafufua mashamba
yao na kuanzisha mapya na Serikali itawasaidia kuhakikisha mbegu bora na
pembejeo zinapatikana.
Kadhalika,
Waziri Mkuu ametoa rai kwa wananchi katika kila mkoa wenye ardhi nzuri
ambayo inastawi zao hilo waanzishe kilimo cha zao mkonge walime na
Serikali itawasaidia bila kujali ni mtu mmoja mmoja, wakulima wa kati na
wakubwa.
“Wakuu
wa wilaya waondoeni Maafisa Kilimo waliopo Ofisini waende vijijini
wakawasaidie wakulima namna nzuri ya kulima zao hili kwa faida, mkonge
ni pesa, Serikali yenu itasimamia. Tunataka mkonge urudi kwenye nafasi
yake. Endeleeni kuwahamasisha walime mkonge, tunataka kila tunapopita
tuone mashamba ya mkonge.”
Ameiagiza
Bodi ya Mkonge kufanya utambuzi wa mashamba na wayarudishe kwa watu
walime. Pia mapori yote makubwa yaliyoko kwenye halmashauri ambayo
hayatumiki nayo wayatambue na waishauri Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi ili nao wamshauri Rais Dkt. Magufuli kwa ajili ya
kugawiwa kwa wananchi waweze kulima.
Katika
mkutano huo, Waziri Mkuu amesema amewahusisha wadau kutoka taasisi
mbalimbali za kifedha na kwamba Serikali imeweka utaratibu
utakaowawezesha wakulima wanaotaka kuboresha mashamba yao waweze kukopa.
“Nendeni Benki ya Kilimo mkachukue mikopo.”
“Zao
la mkonge ni muhimu nchini kwani linawanufaisha wakulima wadogo, wa
kati na wakubwa. Mkonge kwa Tanga ni uchumi kwa wananchi na ni mkombozi
kwa sababu unawawezesha kupata riziki zao. Zao hili hapo katikati
halikuwa na tija, zao hili lilikuwa linalimwa na mikoa zaidi ya 12
lakini sasa limeachwa kwenye mikoa minne tu.”
Waziri
Mkuu amesema kwenye miaka ya 60 Tanzania ilikuwa inaongoza kwa
uzalishaji wa mkonge duniani, ambapo ilikuwa inazalisha tani 235,000
huku mahitaji ya mkonge duniani yakiwa tani 550,000. “Tulikuwa
tunazalisha zaidu ya nusu ya mahitaji ya dunia, leo hii mchango wake
haupo ukiuliza kwa nini hakuna sababu. Serikali imeagizwa na CCM kuwa ni
lazima zao hili lirudi kwenye hadhi yake na litarudi.”
Kufuatia
hali hiyo, Waziri Mkuu ameagiza mikoa yote inayolima zao la mkonge
kuanzia sasa ijipange kwa sababu Serikali imeamua kulifufua zao hilo na
inataka kulirudisha katika nafasi yake, hivyo viongozi wahakikishe
wanaendelea kuwahamasisha wananchi walime kwa wingi.
“Tunataka
mkonge ushamiri, Bodi tumieni vyombo vya habari kuhamaisha wananchi
walime zao hili pamoja na kuwaeleza fursa zitokanazo na zao hilo.
Wawekezaji wetu panueni mashamba, leteni mitambo ya kuchakata mkonge
pamoja na vyote vitokanavyo na mkonge. Nampongeza Mkuu wa Mkoa wa Tanga
amefanya kazi kubwa katika hili.”
Naye,
Naibu Waziri Kilimo, Omar Mgumba ametumia fursa hiyo kumshukuru Waziri
Mkuu kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kusimamia sekta ya kilimo
likiwemo zao la mkonge. “Uadilifu wako na uzalendo wako ulikufanya uunde
kamati ya kuchunguza mali za Bodi ya Mkonge Tanzania na leo hii mali
zao zimerudi.”
“Mheshimiwa
Waziri Mkuu utaingizwa kwenye kumbukumbu za Tanzania kwa kujitoa kwako
katika kuhakikisha zao hili linarudi kama ilivyokuwa awali. Tutafufuka
katika mikoa yote ambayo imeonesha inaweza kulima zao hili la mkonge,
lengo ni kuhakikisha zao hili linarudi kwenye hadhi yake.”
Kwa
upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu amemshukuru Waziri Mkuu kwa kusimamia ajenda za
maendeleo katika mkoa wa Tanga, hususani zao la mkonge.
“Tunashukuru
uliporejesha hadhi ya zao hili.Tutawahimiza wananchi kulima mkonge
kwani tunaona muelekeo na maono ni makubwa sana, Tanga tunajivunia
jitihada hizi za maendeleo, uchumi wa Tanga utakuwa kwa kasi sana.”
Awali,
Mbunge wa Lushoto Rashidi Shangazi alisema wanaishukuru sana Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kuweza kuwarejeshea wananchi mashamba yao.
Nao,
Wakuu wa Mikoa ya Pwani, Morogoro na Kilimanjaro waliishukuru Serikali
kwa kulifufua zao hilo na kwamba wameshaweka mipango ya kuendeleza zao
hilo na wameiomba Wizara ya Kilimo ishirikiane nao kwa kuwasaidia
wakulima katika kuendeleza zao hilo, ikiwemo uandaaji wa mashamba,
uendelezaji pamoja na utafutaji wa masoko. “Wizara ya Kilimo na Wizara
ya Ardhi zitusaidie kutenga maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya
uzalishaji.”
MWISHO
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Post a Comment