WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itahakikisha mali zote za wakulima wa zao la mkonge nchini zinarudishwa mikononi mwao na hakuna mtu yeyote atakayeonewa.

“Tutarudisha mali zote za wakulima na ninawahakikishia hakuna mtu yoyote atakayeonewa, kama tulivyorudisha hizi mali za Bodi ya Mkonge Tanzania tutafanya hivyo hivyo kote bila kumuonea yeyote na kuanzia leo Bodi hii ya Mkonge imethibitishwa kuwa bodi kamili.”

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Juni 1, 2020) wakati akifungua jingo la Bodi ya Mkonge Tanzania zilizopo jijini Tanga. “Mkonge ni fedha Halmashauri wekeni vitalu mzalishe mbegu muwape wananchi bure. Kama unashamba kubwa hujaliendeleza, kulingana na muda uliowekwa, tutalichukua.”

Amesema Serikali imedhamiria kulirudisha zao hilo, hivyo ametoa wito kwa wananchi hususani wa mkoa wa Tanga wajipange katika kuyafufua mashamba yao na kuanzisha mapya na Serikali itawasaidia kuhakikisha mbegu bora na pembejeo zinapatikana.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa rai kwa wananchi katika kila mkoa wenye ardhi nzuri ambayo inastawi zao hilo waanzishe kilimo cha zao mkonge walime na Serikali itawasaidia bila kujali ni mtu mmoja mmoja, wakulima wa kati na wakubwa.

“Wakuu wa wilaya waondoeni Maafisa Kilimo waliopo Ofisini waende vijijini wakawasaidie wakulima namna nzuri ya kulima zao hili kwa faida, mkonge ni pesa, Serikali yenu itasimamia. Tunataka mkonge urudi kwenye nafasi yake. Endeleeni kuwahamasisha walime mkonge, tunataka kila tunapopita tuone mashamba ya mkonge.”

Ameiagiza Bodi ya Mkonge kufanya utambuzi wa mashamba na wayarudishe kwa watu walime. Pia mapori yote makubwa yaliyoko kwenye halmashauri ambayo hayatumiki nayo wayatambue na waishauri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili nao wamshauri Rais Dkt. Magufuli kwa ajili ya kugawiwa kwa wananchi waweze kulima.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu amesema amewahusisha wadau kutoka taasisi mbalimbali za kifedha na kwamba Serikali imeweka utaratibu utakaowawezesha wakulima wanaotaka kuboresha mashamba yao waweze kukopa. “Nendeni Benki ya Kilimo mkachukue mikopo.”

“Zao la mkonge ni muhimu nchini kwani linawanufaisha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa. Mkonge kwa Tanga ni uchumi kwa wananchi na ni mkombozi kwa sababu unawawezesha kupata riziki zao. Zao hili hapo katikati halikuwa na tija, zao hili lilikuwa linalimwa na mikoa zaidi ya 12 lakini sasa limeachwa kwenye mikoa minne tu.”

Waziri Mkuu amesema kwenye miaka ya 60 Tanzania ilikuwa inaongoza kwa uzalishaji wa mkonge duniani, ambapo ilikuwa inazalisha tani 235,000 huku mahitaji ya mkonge duniani yakiwa tani 550,000. “Tulikuwa tunazalisha zaidu ya nusu ya mahitaji ya dunia, leo hii mchango wake haupo ukiuliza kwa nini hakuna sababu. Serikali imeagizwa na CCM kuwa ni lazima zao hili lirudi kwenye hadhi yake na litarudi.”

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu ameagiza mikoa yote inayolima zao la mkonge kuanzia sasa ijipange kwa sababu Serikali imeamua kulifufua zao hilo na inataka kulirudisha katika nafasi yake, hivyo viongozi wahakikishe wanaendelea kuwahamasisha wananchi walime kwa wingi.

“Tunataka mkonge ushamiri, Bodi tumieni vyombo vya habari kuhamaisha wananchi walime zao hili pamoja na kuwaeleza fursa zitokanazo na zao hilo. Wawekezaji wetu panueni mashamba, leteni mitambo ya kuchakata mkonge pamoja na vyote vitokanavyo na mkonge. Nampongeza Mkuu wa Mkoa wa Tanga amefanya kazi kubwa katika hili.”

Naye, Naibu Waziri Kilimo, Omar Mgumba ametumia fursa hiyo kumshukuru Waziri Mkuu kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kusimamia sekta ya kilimo likiwemo zao la mkonge. “Uadilifu wako na uzalendo wako ulikufanya uunde kamati ya kuchunguza mali za Bodi ya Mkonge Tanzania na leo hii mali zao zimerudi.”

“Mheshimiwa Waziri Mkuu utaingizwa kwenye kumbukumbu za Tanzania kwa kujitoa kwako katika kuhakikisha zao hili linarudi kama ilivyokuwa awali. Tutafufuka katika mikoa yote ambayo imeonesha inaweza kulima zao hili la mkonge, lengo ni kuhakikisha zao hili linarudi kwenye hadhi yake.”

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amemshukuru Waziri Mkuu kwa kusimamia ajenda za maendeleo katika mkoa wa Tanga, hususani zao la mkonge.

“Tunashukuru uliporejesha hadhi ya zao hili.Tutawahimiza wananchi kulima mkonge kwani tunaona muelekeo na maono ni makubwa sana, Tanga tunajivunia jitihada hizi za maendeleo, uchumi wa Tanga utakuwa kwa kasi sana.”

Awali, Mbunge wa Lushoto Rashidi Shangazi alisema wanaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuweza kuwarejeshea wananchi mashamba yao.

Nao, Wakuu wa Mikoa ya Pwani, Morogoro na Kilimanjaro waliishukuru Serikali kwa kulifufua zao hilo na kwamba wameshaweka mipango ya kuendeleza zao hilo na wameiomba Wizara ya Kilimo ishirikiane nao kwa kuwasaidia wakulima katika kuendeleza zao hilo, ikiwemo uandaaji wa mashamba, uendelezaji pamoja na utafutaji wa masoko. “Wizara ya Kilimo na Wizara ya Ardhi zitusaidie kutenga maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya uzalishaji.”

MWISHO
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Post a Comment

أحدث أقدم