Desemba 13, 1984 alizaliwa mchezaji wa soka wa kimataifa wa Hispania na klabu ya Villareal Santi Cazorla. Jina lake halisi ni Santiago Cazorla Gonzalez.

Cazorla amekuwa akicheza katika nafasi ya kiungo hususani katika majukumu ya ushambuliaji.

Alizaliwa Llanera, katika jimbo la Asturias nchini Hispania. Alianza maisha ya soka na klabu ya Real Oviedo na baadaye Villareal walimuona miezi michache kabla hajatimiza umri wa miaka 18.

Klabu yake ya zamani iliingia katika ukata wa kifedha hali iliyofanya ishuke daraja mwishoni mwa msimu wa 2002/03.

Real Oviedo ilikwenda moja kwa moja katika Tercera Division (Ligi daraja la tatu).

Kwa upande wake Cazorla alisalia katika timu ya akiba na katika timu ya kwanza alicheza kwa mara ya kwanza Novemba 30, 2003 katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Deportivo de La Coruña akicheza dakika moja baada ya kutolewa kwa Roger Garcia Juyent.

Msimu huo alicheza mara moja akisalia katika benchi. Cazorla alifunga bao lake la kwanza katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Odense Boldklub  katika Uefa Intertoto.


Kwa aufupi Cazorla alianza maisha yake ya soka la kimataifa akiwa na Villareal mwaka 2003, pia aliwahi kutolewa kwa mkopo katika klabu pacha na Villareal ya Recreativo de Huelva.

Msimu wa 2006-07 alitunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa La Liga. Mnamo mwaka 2011 alitua Malaga kwa ada ya euro milioni 21, akiwa huko alijulikana zaidi kutokana na kasi yake, kutandika mikwaju kisawasawa, uwezo wa kubadilisha ladha ya mchezo, na uwezo mkubwa kumiliki mpira.


Baada ya msimu wa 2011-12 Arsenal walimdaka Cazorla kwa ada ya pauni milioni 10 ambapo alikuwa kiungo muhimu kwa msimu wake wa kwanza akitoa pasi za mwisho 12 na msimu huo alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa klabu ya Arsenal.

Jarida la Bloomberg lilimuorodhesha kuwa miongoni mwa wachezaji bora barani Ulaya. Wakati akitua Arsenal kocha Arsene Wenger aliwaleta Lukas Podolski kutoka Ujerumani na Olivier Giroud kutoka Ufaransa.

Bao lake la kwanza dhidi ya Arsenal alilifunga kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Liverpool katika dimba la Anfield.

Pia alifunga hat trick yake ya kwanza dhidi ya Reading na kiwango chake katika mchezo huo kilimpa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi.

Cazorla akiwa Arsenal ndiye aliyekata ukame wa miaka tisa ya kukosa mataji pale alipotandika mkwaju wa mbali na kutwaa taji la FA mwaka 2014.

Majeruhi yalimuandama nyota huyo na ndipo mwaka 2018 alihitimisha safari yake ya kuitumikia Arsenal baada ya miaka sita. Ndipo Cazorla aliporudi Villareal.

Katika timu ya taifa ya Hispania aliitwa kwa mara ya kwanza kwenye mchezo dhidi ya Peru mnamo Mei 2008.

Pia alikuwa miongoni mwa wachezaji waliounda kikosi kilichocheza nusu fainali ya UEFA Euro 2008 na Euro 2012 pia Kombe la Dunia 2014.

Alifunga bao la kwanza la kimataifa katika mchezo dhidi ya Chile na baada ya hapo amecheza mechi 80 akifunga mabao 15.

Post a Comment

Previous Post Next Post