Kwa hakika kuna tofauti kubwa kati ya mwajiriwa na mjasriamali; tofauti hii inahusisha tabia, fikra, maamuzi au hata matendo.
Kuna baadhi ya watu ni wajasiriamali kwa mwonekano lakini kitabia ni waajiriwa; wapo pia wengine ni waajiriwa kimwonekano lakini ni wajasiriamali kitabia.
Ikiwa basi unataka kuwa mjasiriamali, ni muhimu ufahamu tofauti 10 za msingi zilizopo kati ya mwajiriwa na mjasiriamali.
1. Mwajiriwa hupumzika kwenye likizo lakini mjasiriamali hutumia likizo kufanya kazi zaidi
Kwa kawaida waajiriwa hufurahia muda wa likizo kwa sababu ndipo hupata muda wa kupumzika. Hali ni tofauti kwa mjasiriamali kwani hana likizo, na ikiwa ni mjasiriamali aliyeajiriwa, basi atatumia likizo yake kuendeleza mradi au biashara yake.
2. Mwajiriwa hulenga kupanda cheo lakini mjasiriamali hulenga kukuza mradi wake
Mwajiriwa kila mara anafanya kazi kwa bidii ili apandishwe cheo au aongezewe mshahara na marupurupu. Mjasiriamali kila mara huwaza na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza au kuendeleza mradi wake.
3. Mwajiriwa hufikiri pesa ni kila kitu wakati mjasiriamali hufikiri muda ni kila kitu
Mwajiriwa hufikiri kuwa pesa ni kila kitu na ndizo zitakazomwezesha kufikia malengo yake.
Mjasiriamali anafahamu kuwa mafanikio yake yamefungwa kwenye muda, hivyo muda ni wa thamani zaidi kwake na ndio utakaomwezesha kutengeneza pesa zaidi.
4. Mwajiriwa hufuata mpango lakini mjasiriamali hutengeneza mpango
Kwa kawaida mwajiriwa hufuata mapango uliowekwa na mwajiri katika utendaji wake wa kazi. Mjasiriamali huweka mipango na kuwa sehemu ya kutekeleza mipango hiyo.
Mwajiriwa hupangiwa kazi lakini mjasiriamali hujipangia kazi yeye mwenyewe.
5. Mwajiriwa huogopa makosa lakini mjasiriamali hujifunza kutokana na makosa
Mwajiriwa huogopa makosa kwani anafahamu makosa hayo yanaweza kumsababishia kupoteza kazi yake. Makosa kwa mjasiriamali ni shule muhimu ambayo itamwezesha kuboresha kile anachokifanya.
Maisha ya ujasiriamali ni kujaribu vitu vingi na kuchagua kile kinacholeta matokeo mazuri.
6. Mwajiriwa hujikita kwenye kitu kimoja lakini mjasiriamali hujaribu vitu vingi
Mwajiriwa hujikita kwenye kazi au nafasi aliyopewa pekee. Mwajiriwa hana haja ya kujaribu vitu vingi kwani yeye hufanya kile alichopangiwa kufanya.
Hali ni tofauti kwa mjasiriamali kwani yeye hufanya vitu vingi kwa njia ya majaribio ili aone kile kinachofanya vizuri zaidi. Kwa njia hii huweza kuchagua kitu chenye tija zaidi.
Mjasiriamali anaweza kuuza chakula leo, kesho nguo, keshokutwa dawa, n.k. ili tu kubaini kile kinachofanya vizuri zaidi.
7. Mwajiriwa hulipwa kutokana na nafasi yake lakini mjasiriamali hulipwa kutokana na matokeo
Nafasi aliyonayo mwajiriwa ndiyo huamua kiwango cha malipo atakacholipwa. Mwajiriwa akiwa mkurugenzi basi atalipwa kama mkurugenzi; lakini mjasiriamali hulipwa au hupata pesa kutokana na matokeo ya kile anachokifanya.
Ikiwa mradi au biashara ya mjasiriamali haitazalisha faida, basi mjasiriamali husika naye hatapata pesa.
8. Mwajiriwa hutafuta muda sahihi lakini mjasiriamali hatafuti muda sahihi
Mara nyingi hakuna muda sahihi wa mjasiriamali. Mjasiriamali huangalia soko na kuanza kujaribu au kufanyia kazi wazo lake.
Hali ni tofauti kwa mwajiriwa, kwani yeye hutafuta muda sahihi wakufanya maamuzi na matendo mbalimbali katika taasisi au ofisi aliyoajiriwa ili kulinda ajira yake.
9. Mwajiriwa huchukua hatari chache lakini mjasiriamali anaishi nazo
Kwa hakika ujasiriamali ni swala lenye hatari au changamoto nyingi, kukubali kuwa mjasiriamali ni lazima uwe umekubali kukabili changamoto na hatari mbalimbali.
Unaweza kuzalisha bidhaa zikakosa soko au ukakabiliwa na changamoto nyingine kama vile kukosa mtaji au mzunguko mdogo wa pesa.
Mwajiriwa hana haja ya kujali sana juu ya hatari kadhaa, kwani kuna watu tayari wapo kwa ajili ya kufanya maamuzi mbalimbali ya taasisi au kampuni iliyomwajiri.
10. Mwajiriwa anafuata ratiba iliyowekwa lakini mjasiriamali anajiwekea ratiba yeye wenyewe
Kauli kama vile “Muda wa kazi umefika” “Muda wa kazi umekwisha” ni kauli unazoweza kuzisikia tu kwa waajiriwa. Mjasiriamali hana muda wa kazi, anatakiwa kufanya kazi kwa bidii kila wakati na kila mahali hadi pale atakapopata matokeo chanya.
Hata hivyo mwajiriwa hana uhuru alionao mjasiriamali, kwani mjasiriamali anaweza kufanya kazi muda wowote au kupumzika muda wowote lakini mwajiriwa anatakiwa afuate ratiba ya kazi kila wakati.
Neno la mwisho
Kwa hakika kuna tofauti kubwa kati ya mwajiriwa na mjasiriamali. Kwa ujumla tunaweza kusema ujasiriamali ni jambo zuri zaidi ambalo hukuongezea pia uwezo wako wa kufikiri, kutenda na hata kufanya maamuzi.
إرسال تعليق