Na Said Mwishehe,Michuzi TV


WADAU wa maendeleo kutoka asasi za kiraia zipatazo 28 nchini Tanzania wamekutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata mrejesho wa wenzao wapatao 20 waliokwenda nchini Marekani kushiriki mkutano wa Jukwaa la Kisiasa la hali ya juu la malengo ya maendeleo endelevu.

Kupitia jukwaa hilo asasi hizo zimepata nafasi ya kuwasilisha ripoti yao kuhusu malengo ya maendeleo endelevu huku wakieleza kufurahishwa na hatua ya Serikali ya Tanzania kuahidi kusimamia na kutekeleza malengo yote 17 yaliyoko kwenye mkakati wa maendeleo endelevu.

Akizungumza na Michuzi TV pamoja na Michuzi Blog leo Julai 31 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Forumcc Angela Damas amesema jumla ya ujumbe wa watu 20 walikwenda nchini Marekani katika jukwaa hilo kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo endelevu.

"Leo hii tumekutana hapa kwa ajili ya kupata mrejesho kutoka kwa wenzetu waliotuwakilisha Marekani katika Jukwaa la Kisiasa la Hali ya Juu la Maendeleo Endelevu ambalo limefanyika kwa wiki mbili.

"Katika mkutano huo nchi yetu nayo imepata nafasi ya kuwasilisha ripoti yake ya namna ambavyo inatekeleza malengo ya maendeleo endelevu.Kwetu ni faraja kuona nchi inawasilisha ripoti lakini wakati huo huo asasi za kijamii nazo zimepata nafasi hiyo na kwa pamoja tunaamini tutasonga mbele,"amesema Damas.

Pia amesema watatumia nafasi hiyo kuangali ni kwa namna gani asasi za kiraia zinaweza kushiriki kikamilifu kuhakikisha malengo ya maendeleo endelevu yanafanikiwa.

Ameongeza wao ni mara kwa kwanza kushiriki na ripoti iliyowasilishwa ilihusu malengo sita tu kati ya malengo 17 yaliyowekwa na kufafanua kila baada ya miaka mitatu kunakuwa na kikao cha kuwasilisha ripoti.
Alipoulizwa iwapo malengo hayo yamefanikiwa , amejibu ni ngumu kupima kwa haraka na kueleza kama kuna mafanikio au laa lakini kikubwa kuna hatua nzuri ambazo zinaonekana, hivyo ni kuunganisha nguvu ya pamoja.

"Hivyo hakuna jibu la moja kwa moja, binafsi naweza kueleza hata ripoti hii iliyowasilishwa inatoa tu muelekeo wa awali jinsi gani tunaendelea kuweka nguvu katika kufikia malengo yaliyowekwa,"amesema Damas.

Hata hivyo amesema kwenye mkutano wa jukwaa hilo, kuna baadhi ya changamoto ambazo zimeonekana na kutoa mfano nchi za Afrika Kusini na Namibia zinajihusisha zaidi na uchimbaji madini na shughuli za viwanda.

"Nchi hizo licha ya uchumi kukua bado hali halisi ya maendeleo haiendani na huduma za kijamii kama elimu na afya. Hivyo kuna kila sababu ya kuweka mikakati ya kuleta maendeleo ya pamoja katika maeneo yote na sisi asasi za kijamii tunalo jukumu la kushirikiana na Serikali zetu kuleta maendeleo,"amesema Damas.

Wakati huo huo amesema pamoja na ripoti yao ambayo wameiandaa kwa kipindi cha mwaka mmoja, wapo kweny mchakato wa kufanya uchambuzi na kisha kuwasilisha serikalini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu -UN Tanzania Reynald Maeda ambaye pia anatoka kwenye Waratibu wa Jukwaa la Maendeleo Endelevu nchini amesema katika jukwaa hilo nchi yetu ya Tanzania nayo ilikuwa inatoa ripoti yake kuhusu utekelezwaji wa malengo ya maendeleo endelevu kuanzia tulipoanza na tulipo sasa.

"Maoni yetu asasi za kiraia nayo yalijumuishwa kwenye ripoti ya nchi na kuna asasi nyingi ambazo zimeshiriki.Malengo sita ndio yaliwakilishwa kwa mwaka huu.

"Na jambo kubwa zaidi ni ushirikishwaji na kutoacha mtu nyuma, kwani malengo ni kutoacha mtu nyuma kwenye maendeleo endelevu,"amesema Maeda.
 Baadhi ya viongozi wa za kiraia nchini Tanzania wakiwa wameshika ripoti yao ambayo  pamoja na mambo mengine anaelezea kuhusu makongo ya maendeleo endelevu.Ripoti hiyo wameizundua rasmi leo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha kupata mrejesho kwa wenzao waliorejea nchini wakitoa nchini Marekani kwenye Jukwaa la Kisiasa la hali ya juu la malengo ya maendeleo endelevu
 Wadau wa maendeleo kutoka asasi za kiraia wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati walipokutana kupata mrejesho wa wenzao waliowawakilisha nchini Marekani  katika Jukwaa la Maendeleo la hali ya juu la malengo ya maendeleo endelevu
 Baadhi ya wajumbe wa asas za kiraia waliofika kupata mrejesho  wakiwa katika picha ya pamoja
 Sehemu ya wajumbe wa asasi za kiraia wakifuatilia mrejesho unaotolewa na wenzao waliofika nchini Marekani katika mkutano wa jukwaa la kisiasa la hali ya juu la malengo ya maendeleo endelevu
Mkurugenzi wa Programu kutoka FORUMCC   Angela Damas akifafanua jambo wakati wa mkutano huo

Post a Comment

أحدث أقدم