Na Charles James, Michuzi TV

Vijana nchini wameaswa kuwa wazalendo Na wabunifu ili waweze kufikia malengo yao na kuacha kuwa tegemezi huku wakisubiri kuajiriwa na badala yake wajikite katika kujiajiri wenyewe.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Sehemu ya Utumishi na Utawala wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Veronica Ndavo wakati wa kuwaaga wanafunzi wa kitivo cha Tiba wa Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyoandaliwa na wanafunzi hao ambao ni wanachama wa CCM, Ndugu Veronica amewaasa vijana hao ambao ni wataalamu wa afya, wafamasia, wauguzi na maafisa wa mazingira na matibabu kuhakikisha wanatumia elimu waliyopata katika kukitumikia Chama chao, jamii inayowazunguka pamoja na Serikali.

" Nawapongeza sana kwa kuhitimu niwasihi mnapoelekea mtaani msibague kazi lakini pia hizo kazi zisishushe utu wako, nendeni mtaani mkafanye kazi ili tumsaidie Rais wetu katika kufikia uchumi wa viwanda.

" Niwapongeze pia kwa kukuza kipato cha tawi lenu la Chama kutoka Shilingi Laki Moja hadi kufikia Laki Sita, naahidi kuwapa ushirikiano na nitatoa mifuko ya Saruji yenye thamani ya Shilingi Laki Tatu, pamoja na vitendea kazi vyenu vya Chama zikiwemo Kompyuta ambayo nitaikabidhi hapa leo. Lengo letu ni kuona hamkwami kwenye shughuli zenu za Chama," amesema Veronica.

Aidha Veronica amekabidhi kiasi cha Shilingi Laki mbili kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya CCM ya Kata ya Ng'hong'hona ambayo kwa asilimia kubwa imekua ikitumiwa na wananchi hao ambao ni wanachama wa Chama hicho.

" Niwatake pia mkawe msaada mkubwa wa Chama chetu kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaokuja hivi karibuni, Rais wetu Dk John Magufuli amefanya kazi kubwa za kimaendeleo zawadi pekee tunayoweza kumpa ni ushindi wa kishindo wa CCM kwenye chaguzi hizi. Nyie ni vijana kaonesheni thamani yenu na nguvu yenu ndani ya Chama kwa kukisaidia kushinda uchaguzi huu," amesema Veronica.

Nae Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Diana Madukwa amemshukuru Bi Veronica kwa kujitoa kwake katika kuwachangia vijana hao na kuahidi kuendelea kuwalea wanafunzi wanaobakia katika maadili ya kiuongozi na yenye utumishi ndani ya Chama.

" CCM Wilaya tutaendelea kuwa bega kwa bega na vijana wanaohitimu na wale wanaobaki, tutawalea kichama ili kutimiza ndoto zenu za kuwa viongozi wakubwa kisiasa na kiserikali lakini zaidi kuwa wanachama waaminifu na wazalendo kwa Nchi yao," amesema Diana.
 Mkuu wa Utumishi na Utawala aa Chama cha Mapinduzi, Veronica Ndavo akikabidhi Kompyuta kwa uongozi wa wanafunzi wa kitivo cha afya chuo kikuu cha Dodoma ambao ni wanachama wa CCM
 Mkuu wa Sehemu ya Utumishi, Utawala wa Chama cha Mapinduzi, Veronica Ndavo akizungumza na wanafunzi wa Kitivo cha Afya chuo Kikuu cha UDOM ambao ni wanachama wa CCM wakati wa hafla ya kuwaga wanafunzi wa Jumuiya hiyo wanaohitimu masomo yao
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma, Diana Madukwa Akizungumza na wanafunzi wanachama wa CCM kutoka kitivo cha Afya chuo Kikuu cha UDOM wakati wa afya ya kuwaaga wanafunzi wanaohitimu masomo yao

Post a Comment

Previous Post Next Post