Maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Dar es
Salaam yanakwenda vizuri ambapo ujenzi wa magati 2 kati ya 7 yaliyopo
umekamilika na kuanza kupokea meli kubwa za mizigo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema mradi wa ujenzi wa
magati hayo utakaogharimu takribani shilingi Trilioni moja utaiwezesha Bandari
ya Dar es Salaam kuongeza ufanisi kwa kuongeza kasi ya upakuaji na upakiaji wa
mizigo na kupokea meli yoyote duniani zikiwemo meli kubwa za kizazi cha saba (7th Generation).
Mhandisi Kakoko amefafanua kuwa kazi
inayoendelea imewezesha kukamilika kwa ujenzi katika gati namba 1 na gati namba
2 ambazo zimeongezwa kina kutoka mita 8 hadi kufikia kati ya mita 15 na 19,
kina ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na kina kinahitajika kwa meli kubwa zaidi
ambacho ni mita 12.
Aidha, Mhandisi Kakoko amemshukuru Mhe. Rais
Magufuli kwa kutilia mkazo ujenzi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuamua kujenga
gati nyingine ya magari iitwayo RORO ambayo itaiwezesha bandari hiyo kupokea
meli hata 2 kwa mpigo zenyewe uwezo wa kuchukua magari 10,000 ikilinganishwa na
uwezo wa kuchukua magari 200 kabla ya mradi huo.
“Sasa maana yake nini, magari ni kati ya
shehena inayoingiza tozo zaidi, kwa magari pekee yake tunaweza kukusanya tozo
mara 2 au mara 3 ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, ndio maana tunamshukuru
Mhe. Rais Magufuli kwa kutuongezea hiyo gati ya RORO.
Kwa hiyo faida ya kwanza tunaipata katika
kuongeza kina kwa maana meli kubwa zitaingia kwa mara moja, na kuna watu
wamekuwa wakiona kuna Kijiji cha meli zinazosubiri kuingia bandari kushusha
mizigo, hiyo haiwezi kuwepo tena” amesema Mhandisi Kakoko.
Mhandisi Kakoko amesema juhudi hizo
zinakwenda sambamba na uboreshaji eneo la nyaraka (clearing) kupitia serikali mtandao ili kuondoa mianya ya
udanganyifu ambao husababisha upotevu wa mapato.
“Sasa tutaweza kupata moja kwa moja Bill of
Lading na hivyo kuondokana na baadhi ya wafanyabiashara au waagizaji mizigo
ambao hudai makontena yana mitumba wakati ndani mna magari” amesema Mhandisi
Kakoko na kubainisha kuwa uwekaji wa mfumo wa nyaraka unakwenda sambamba na
uwekaji wa mitambo ya ukaguzi (scanner).
Amesema baada ya kukamilika kwa gati namba 1
na gati namba 2, ujenzi kwa sasa unaendelea katika gati namba 4 ambayo
inakaribia kukabidhiwa TPA na gati namba 5 ambayo uchorongaji unaendelea.
Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa
ujenzi wa gati namba 3 na gati namba 4, ujenzi huo utaendelea kwa gati namba
5,6 na 7 na baada ya hapo kazi itaendelea kwa magati ambayo yapo chini ya Kampuni
ya Kimataifa ya Huduma za Makontena Bandarini (TICTS) ambayo tayari Serikali ya Awamu ya Tano imeshafanya
mazungumzo ya kurekebisha mkataba na sasa mrabaha unaolipwa ni mara 2
ikilinganishwa na zamani.
Mhandisi Kakoko amesema pamoja na kujenga
gati hizo, Serikali pia inanunua mitambo mikubwa ya kupakulia na kupakia mizigo
na hivyo kuongeza kasi na ufanisi zaidi wa bandari.
Kufuatia juhudi hizo amesema sasa bandari ya
Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kutumia vizuri faida yake ya kijiografia
kukabiliana na ushindani wa bandari zote zilizopo katika ukanda wa bandari ya
Hindi na kuwa lango bora na muhimu kwa nchi za Afrika.
Mhandisi Kakoko amesema kazi hii ya
uboreshaji wa Bandari a Dar es Salaam iliyopaswa kufanyika miaka 30 iliyopita
imesababisha Tanzania kupoteza kiasi kikubwa cha mapato na kwamba kutokana na
uboreshaji huu na hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imechukua, TPA
itaendelea kuongoza katika utoaji wa gawio.
Ameahidi kuwa mwaka huu TPA inatarajia kutoa
gawio la kati ya shilingi Bilioni 150 na shilingi Bilioni 200 na kwamba miaka
michache ijayo TPA kwa kushirikiana na wadau wengine wa bandari watakuwa na
uwezo wa kuzalisha fedha za kugharamia bajeti nzima ya Serikali ambayo ni
takribani shilingi Trilioni 30 kwa mwaka.
Halikadhalika Mhandisi Kakoko amesema kazi
ya ujenzi wa bandari pia inaendelea katika Bandari ya Mtwara na ujenzi katika
Bandari ya Tanga utaanza mwezi huu (Agosti 2019)
Post a Comment